AFRICA MAGIC SWAHILI WAFANYE MABADILIKO



Kuanzishwa kwa Channel ya AMS (Africa Magic Swahili) kulikuwa sehemu ya mabadiliko makubwa katika tasnia ya filamu hapa nchini. Hii ina maana filamu zetu hazitaishia kuonyeshwa na ITV, Channel 10, Channel 5, TBC 1, C2C, Clouds TV, Mlimani TV, na kahdalika.
Mabadiliko hayo sio kusmimuliwa kupitia redio zetu pekee, bali hatua kubwa kwa waigizaji wenyewe na kazi zao. Pia manufaa kwa Africa Magic Swahili kwa kufanya biashara nzuri na yenye tija kwa nchi za afrika mashariki.
Tunajua kuwa fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kufikisha ujumbe wake. Vilevile Africa Magic Swahili ni sehemu ya jamii kwahiyo kujitokeza hadharani kulikuwa na maana wamejiandaa kukosolewa, kusifiwa na kukubalia kuwa wabunifu zaidi.
Kuna mambo mazuri sana katika Africa Magic, pia kuna mambo mengine sio mazuri kabisa kwakuwa imekuwa kero zaidi. Bahati nzuri suala hilo halipo kwa wapenzi wa filamu nchini pekee, bali hata kwa waigizaji.
Waigizaji wanapofika mahali wanakosoa mwenendo wa Africa Magic Swahili, ambayo mwanzoni walishangilia ujio wake, basi ujue kuna tatizo katika tasnia ya filamu na shime wahusika wanatakiwa kufanyia kazi.
Mimi nimekuwa mdau mkubwa katika Channel hiyo, ninaweza kusema kifupi tu, siridhishwi na kazi zinazoonyeshwa. Sio rahisi kuwananga Africa Magic kuwa hawajali au hawaelewi maana ya kuwa makini.
Lakini lazima wabadilike zaidi na wafanye jitihada kuwashawishi waigizaji wakubwa kuwasilisha kazi zao kituonni hapo. Kwanini ninasema hivi?
Hivi karibuni mwigizaji hodari wa filamu nchini Jacob Steven(JB) amelalamikia kituo cha Africa Magic kutoa malipo kidogo kwa kazi zinazowasilishwa.
JB anadai kuwa malipo madogo yanayotolewa na kampuni ya Maultichoice kutokana na kazi zao zinazoonyeshwa Channel ya Africa Magic Swahili inasababisha baadhi yao waache kupeleka kazi zao katika channel hiyo.
JB alikaririwa akisema, baadhi ya filamu zinazoonyeshwa Africa Magic Swahili hazina ubora wa kutosha. JB anaongeza kuwa matokeo yake watazamaji wa hapa nchini na nje wanadhani filamu za Tanzania ni nyepesi au rahisi mno kadiri wanavyoziona, kumbe kuna filamu bora zaidi hazipelekwi Africa Magic Swahili kwakuwa malipo ni madogo sana.
JB alikaririwa akisema, “kwanza kabisa leno la kuanzishwa kwa stesheni ile ilikuwa ni kukikuza kiswahili matokeo yake inaonekana kwenye nchi za afrika mashariki ambazo baadhi wanakijua Kiswahili hivyo ili iwe na maana iende mbali ivuke ndio lengo la kukitangaza Kiswahili litatimia”. Aidha, alikaririwa pia akisema; “kwa malipo wanayolipa si rahisi kupata kitu ambacho wamekusudia ili waweze kuzitangaza filamu za Tanzania ni bora wakaongeza mapato lakini kwa ilivyo sasa ni sawa na kutoa bure ingawa ni mkataba na makubaliano maalumu lakini bado ni kidogo sana”.
Bahati nzuri ni kwamba Ofisa Uhusiano wa Multchoice, Barbara Kambogi ameeleza kuwa suala hilo ni miongoni mwa changamoto zinazofanyiwa kazi na akaongeza kusema masafa ya stesheni hiyo yanafanyiwa marekebisho ili yaweze kufika nchi zingine.
Kwanza namuunga mkono JB kwa msimamo mkali, na pili tumuunge mkono Bi Kambogi kwa uungwana wake kukiri na kusema mabadiliko yatakuja tu katika masuala hayo. Jambo muhimu hapa ni Multchoice kuelewa kuwa idadi ya watumiaji wa huduma ya kulipia ya DSTV imekuwa kubwa, sababu filamu za Tanzania zinapendwa na watanzania wenyewe.
Kwahiyo hatua ya watanzania kupenda kumiliki huduma za DSTV maana yake inatakiwa Africa Magic Swahili iende kwa wakati katika ushindani wa soko la filamu. Changamoto nyingine ni kulipia huduma za DSTV kwa kutumia dola badala ya shilingi. Hii ni changamoto kubwa kuliko zote,
Maana suala la mwigziaji wa filamu JB unaweza kumwita na kutengeneza mkataba mnono naye akakubali kisha kuchukua kitita chake. Lakini suala la kulipia huduma hiyo kwa dola badala ya shilingi ni tatizo jingine kubwa mno.
Katika suala filamu lazima tukiri bado hatujaona filamu bora tunzoona mitaani zikionyeshwa Africa Magic Swahili. Baada ya kujiuliza sana nadhani sasa JB anatupatia majibu na kuifahamisha jamii kuwa kuna unyonyaji na lazima ufanyiwe kazi.
Pengine Multchoce inashindw akugundua jambo moja muhimu sana. Multchoice inaweza kuwachukua waigizaji fulani na kuingia nao mkataba ili filamu zao zionyeshwe katika stesheni yao, yaani kama unaona JB ana soko kubwa katika filamu basi yeye anatafutwa na kupewa mkataba mnono ili filamu zake zinapotengenezwa moja kwa moja zinaingia kwenye rada za Multchoice badala ya kungojea watu wanazungumziaje au idadi ya w apenzi wa filamu yake wanavyojisikia.
Au Multchoice inaweza kujiingiza katika soko la filamu kwa kumiliki waigizaji wake kwa mkataba maalumu. Waigizaji hao watakuwa wakifanyia kazi katika kampuni yao, wachukua mfano wa Sony, 20th Century Fox, Paramount Pictures, SpyGlass, au Universal Channel.
Hiyo ni mifano midogo tu, kwani itasaidia kuepuka malalamiko kama hayo. Pia Multchoice inapokuwa na waigizaji wake maana yake inakuwa na uwanja mwingine wa kuingia mikataba na waigizaji wan je ya kampuni yao.
Ni rahisi, ikiwa utafiti wa kibiashara na masoko utafanywa. Vinginevyo Africa Magic Swahili inapaswa kuwasikiliza waigizaji na ipange kiwango bora cha malipo kwa waigizaji bora na filamu bora, sio kila filamu ionyeshwe Africa Magic Swahili.

Na Markus Mpangala
[Mdau Wetu]
Asante!

Posted by bongofilmdatabase on 11:47 AM. Filed under , , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for AFRICA MAGIC SWAHILI WAFANYE MABADILIKO

Post a Comment

LETS HOOK UP

.

.
.
slide

SIRI YA MTUNGI PHOTO CAPTION


Recently Commented

ALBUM YA BONGOFILM

SIMULIZI ZILIZOBAMBA KWENYE KURASA ZA KIJAMII

TAKE ONE -HBABA NA FLORA INTERVIEW

2009 Bongofilmdatabase. All Rights Reserved. - Designed by Oscar kwa ushirikiano wa SimplexDesign