MCHAKATO WA KULIPAMBA TAIFA NA SANAA ZA NYUMBANI WAANZA
mpya, slide 11:30 PM
Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za ufundi nchini liko
mbioni kuzindua kampeni ambayo italenga kujenga msukumo wa kulipamba taifa na
Sanaa mbalimbali nyumbani.
Akizungumza wiki hii kwenye
kikao cha awali cha maandalizi ya kampeni hiyo kilichofanyika BASATA jijini Dar
es Salaam, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Ghonche Materego alisema kuwa, lengo
ni kuhakikisha maeneo ya miji, majiji, manispaa, ofisi, mahoteli na mazingira
mbalimbali yanaona umuhimu wa kununua sanaa za nyumbani na kuzitumia kupamba.
“Hatujapamba kabisa kwa
sanaa zetu, maeneo mengi ya miji, kuta za maofisi, nyumba zetu na kadhalika ni
matupu. Ni wazi kunahitajika msukumo wa pekee katika kuhakikisha
tunaipendezesha nchi yetu kila mahali na Sanaa mbalimbali” alisisitiza
Materego.
Kwa mujibu wa
Materego, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa vipaji vingi na yenye historia ya pekee
katika Sanaa za Ufundi hivyo ingetarajiwa sanaa hizo kupamba kwa wingi miji,
fukwe, maofisi, shule, majumba, mahoteli na maeneo mbalimbali.
“Sasa kama wasanii
tuingalie nchi yetu, tujiweke mbele katika kuangalia namna ya kuipamba kwa
Sanaa zetu.Tukichelewa itapambwa na Sanaa za nje” aliongeza Materego.
Alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete kwa kutilia mkazo mapambo ya
Sanaa za nyumbani na kutoa wito kwa ofisi zingine za umma kuiga mkakati huo
kwani ni aibu kutumia sanaa za nje kupamba.
“Mara baada ya Rais
Kikwete kuingia Ikulu kulifanyika ukarabati, maonesho ya Sanaa za ufundi
yaliandaliwa ili kupata Sanaa za kuipamba Ikulu yetu, hili ni jambo la faraja
kwamba, na sisi tuna pa kuanzia” alisema Materego.
Alitaja faida za
kampeni ya kulipamba taifa na Sanaa za nyumbani kuwa ni pamoja na kutanua soko
la kazi za wasanii, kulipendezesha taifa
na kazi mbalimbali za mikono, kuwathamini wasanii na nyingine nyingi.
Nchi ya Tanzania ni
miongoni mwa mataifa yanayovuma kwa Sanaa za Ufundi duniani kama michoro,
vinyago, ususi na kadhalika lakini pamoja na utajiri huo bado Sanaa hizi
hazijapewa nguvu kubwa ndani ya mipaka.
Captions
1.
Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche
Materego akisistiza jambo kuhusu haja ya kulipamba taifa na kazi za Sanaa za
nyumbani kwenye kikao cha awali cha maandalilzi ya kampeni hiyo. Kulia kwake ni
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini Adrian Nyangamalle.
2.
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi
Bw.Nyangamalle akichangia kuhusu mikakati ya uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo
kama ikifanikiwa italipendezesha taifa na kazi mbalimbali za mikono.
3.
Wajumbe waliohudhuria kikao hicho
wakifuatilia mchango wa mmoja wa wajumbe kwa makini.