MPANGO WA SERIKALI KWA WASANII NI MAZINGAOMBWE!
mtandao 2:08 PM
Mara nyingi kumekuwa kukitolewa takwimu fulani kuhusu kundi husika bila utafiti, leo sisi tunapenda kuongelea tasania ya filamu Swahiliwood ambayo si rasmi huku taasisi zinazohusika na tasnia hiyo zikiwa makini tu kuhakikisha zinavuna fedha bila kutengeneza mazingira ya kufaidisha upande unaozalisha kazi hiyo.
Kwa mfano hivi sasa tasnia ya filamu inajikuta inakabwa katika taasisi tatu ambazo ni Bodi ya Ukaguzi wa filamu ambayo ipo kisheria, kuna COSOTA ambayo ni tatizo kubwa kwa wasanii, kuna hawa BASATA nao eti wanahusika na filamu, tatizo la taasisi hizi ni pale yanapotekea matatizo maamuzi yao yanatia shaka, hivi kweli mwizi wa kazi za wasanii hajulikani?
Ignas Mkindi ni mkubwa mdau wa filamu kutokana na kuwemo katika tasnia kwa zaidi ya miaka kumi kama Mwongozaji (Director), Mwandika mswada (scriptwriter), Mtayarishaji (Producer) na Mkuu wa sakafu (Production Manager) katika filamu zaidi ya ishirini na tano zikiwemo AUGUA (2001), FIKIRI (2004), SANDA NYEUSI(2008), BESTMAN (2009), WRONG DECISION (2010), ASALI CHACHU (2010) na DIANA (2012).
Pia ni mwanaharakati katika maendeleo ya tasnia ya filamu kwa muda wote huo zikiwemo harakati za kutoa mafunzo kwa waigizaji DDC Magomeni Kondoa (2000 – 2004), Mafunzo ya uandishi wa miswada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2007) na harakati za mchakato wa marekebisho ya sheria ya filamu na uanzishwaji wa shirikisho la filamu kupitia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu (2009).
Usimamizi wa tasnia ya filamu
Hadi muda huu sheria inayosimamia tasnia ya filamu ni Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976 (namba 4) iliyosainiwa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo iliunda Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.
Hata ilipoundwa sheria namba 23 ya mwaka 1984 iliyoanzisha BARAZA LA SANAA LA TAIFA (BASATA) kwa kuunganisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa na kuitambua Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1974, haikuifuta sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya 1976 wala haikuwa na lengo la kuipa BASATA nguvu ya kusimamia filamu kama wanavyojaribu kufanya hivi sasa.
Pamoja na tafsiri nyingine za kazi za sanaa katika sheria iliyounda Basata kipengele cha 2(a)(iv), kazi ya sanaa inayosimamiwa na BASATA imetafsiriwa kama ‘Picha ambazo hazikutengenezwa kwenye mashine ya picha za filamu’
Filamu ni zaidi ya sanaa, ni suala mtambuka ambalo linahusisha taaluma nyingi, na waigizaji ambao ni wasanii ni sehemu ndogo tu ya tasnia ya filamu ila huwa wanaonekana kuwa na nguvu sana kwa kuwa ndiyo wanaoonekana. Wasanii wengine katika tasnia ya filamu ni wabunifu wa mavazi, warembaji na wapambaji wa sehemu za kuchukulia picha.
Kwa kuwa wakati inatengenezwa sheria hiyo ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka 1976 hakukuwa na televisheni, wasambazaji wala maduka ya kukodisha mikanda ya video, sheria hiyo imejikita zaidi katika utengenezaji wa filamu na maonyesho ya filamu hadharani (kwenye majumba ya sinema).
Kwa juhudi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na dhamira aliyokuwa nayo Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kwa wakati huo, Mheshimiwa Kapteni Mstaafu George Mkuchika, wizara ikaanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo iliyopitwa na wakati ili iwe SHERIA YA MAMLAKA YA FILAMU.
.
zoezi hilo lilisimamiwa vema na Mama Rose Sayore akishirikiana na katibu wa Bodi ya Ukaguzi wa filamu kwa wakati ule Lily Beleko, mwanasheria wa Wizara Patrick Kipangula pamoja na wafanyakazi wa Bodi tena wakisisitiza kwa wasanii wawaite wasanii wengine kwa ajili ya mchakato huo.
Huo ndiyo ulikuwa ufumbuzi wa kweli wa matatizo katika tasnia ya filamu.
Nini kilitokea?
Sisi kama wadau tuliitwa mwezi Mei, 2009 kujadili marekebisho ya sheria hiyo kwa siku mbili na kutoa mapendekezo yetu. Hatua iliyofuatia ilikuwa iwe ni majadiliano ya wadau wa ndani ya serikali kisha ipelekwe katika baraza la mawaziri kabla ya kupelekwa bungeni.
.
Pia siku ya tatu tulifanya uchaguzi wa kamati ya wadau kuangalia namna ya mchakato wa kuunda Shirikisho la Filamu Tanzania (SHIFITA) kauli mbiu ikitwa ‘Swahiliwood’ ili liweze kuwaunganisha wadau wa filamu kusukuma upatikanaji wa sheria hiyo.
Sitazungumzia mvurugano uliotokea kati ya BASATA, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na wasanii wa filamu kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa shirikisho kwa kuwa siyo muhimu kwa sasa kutokana na ukweli kuwa tayari kuna Shirikisho la Filamu Tanzania.
Siku ya siku kwa kuwatumia wasanii hao hao ambao hata hawakuwa na muda wa kuangalia sheria ya awali ilikuwa inampa nani mamlaka ya kusimamia filamu kisheria waliingia mkenge na hatimaye shirikisho liliundwa chini ya BASATA, lakini katika jambo la ajabu kushinda yote BASATA hao hao wameshindwa kumaliza mgogoro unaoendelea kati ya Shirikisho hilo TAFF na Bongo Movie Clubhiyo siyo siri tena ugomvi upo tena mkubwa.
Ila kikubwa ninachokiona ni kuwa, kuna baadhi ya watendaji wa serikali wananufaika na mvurugano wa kisheria uliopo katika usimamizi wa tasnia ya filamu ndiyo maana wanakwamisha marekebisho ya sheria ya filamu na kuishauri serikali mambo ambayo hayawasaidii asilimia kubwa ya wadau wa filamu.
Waathirika ni kina nani?
Wasanii mastaa siyo waathirika sana wa hali iliyopo kwa maana huwa hawaigizi mpaka walipwe fedha wanazotaka, na hata wakiandaa filamu, wengi wao wanakuwa washauza haki miliki kwa wasambazaji ila wao ndiyo wanapata fursa ya kusikilizwa sana na viongozi wa juu wa serikali kwa kuwa ndiyo wanaoonekana sana kwenye vioo (screen). Siyo vibaya kutokana na uelewa wa viongozi wa juu kuhusu filamu ila je, wataalamu wa filamu walioajiriwa na serikali wanafanya nini?
Waathirika wakubwa ni watayarishaji waliowafanya hawa mastaa wawepo kisha wakawekwa pembeni na mfumo wa wasambazaji kuwapa fedha moja kwa moja waigizaji wawatengenezee filamu ambazo wamiliki wanakuwa wasambazaji. Siwalaumu wasambazaji kwa sababu wanafanya biashara kutafuta faida, lawama ni kwa watendaji wa serikali ambao wanawafumba macho wasanii wasioelewa kuwa maadui zao ni wasambazaji kumbe wao ndiyo maadui.
Ukitaka kuuthibitisha ukweli huu kaangalie COSOTA kama kuna zaidi ya asilimia kumi za filamu za mastaa zinazomilikiwa na waliozitengeneza au ongea na watayarishaji wakongwe kama Amri Bawji wa Tanga, Sultani Tamba na Jimmy Mponda (Jimmy Master).
Waathirika wengine ni maelfu ya wasanii wachanga wanaohangaika kutoka na kuigizishwa kwa malipo kidogo katika filamu hizo za wasambazaji zinazotengenezwa na wasanii mastaa.
.
Hitimisho
Tunaishauri Serikali na watendaji wao kufanya utafiti wa kina kwa kuwa na wadau wenye uzoefu na uelewa wa tasnia hiyo kwa undani kuliko kuwatumia wasanii kwa muonekano wao katika filamu wakaamini kuwa wanaweza kupata taarifa sahihi kuhusu mustakabali wa tasnia ya filamu na maslahi kwa wahusika.
Ulimwenguni kote wizi wa kazi za wasanii upo lakini unamalizwa na mfumo makini na thabiti kupitia vyombo husika vinavyolinda haki za wamiliki wa halali wa kazi hizo si kama ilivyo kwa COSOTA na BASATA inapotokea wizi kusimama kwa aliye nacho, hali ambayo ujenga chuki na watu kukosa imani na taasisi husika.
Sehemu kama Hollywood filamu haiingii sokoni kwa kuuzwa Dvd! Lazima kazi hiyo ionyeshwe katika majumba ya Sinema na Dvd au kitu chochote utolewa kwa maagizo maalumu ya kibiashara, hapa kwetu hatuna wasambazaji wa filamu bali kuna wanunuzi wa haki za wasanii na watayarishaji jambo ambalo Serikali wanatakiwa kuliona.
Leo hali ya ngoma za asili ipoje hapa nchini? Na msimamizi wa utamaduni ni nani? Tunakimbilia filamu tutaiweza wakati kama taasisi imeshindwa kusimamia utamaduni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa ngoma za asili na utamaduni unalindwa kwa gharama yoyote, hivi sasa matangazo mengi yanatumia muziki kutoka nje hawa wasanii mnaotaka kodi yao wanaipataje hiyo fedha? BASATA mpo kweli?
Kutokana na hali hiyo nadhani mtakubaliana nasi kuwa SERIKALI KUANZISHA STEMPU NI NJIA YA KUJIONGEZEA MAPATO YENYEWE NA SIO KUWASADIA WASANII.
CHANZO; FILAMU CENTRAL
ASANTE!