BISHOP HILUKA ; MATATIZO HAYA MPAKA LINI?

SEKTA ya filamu ni moja ya sekta ambazo zimezongwa na matatizo makubwa. Tathmini nyingi zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika zinabaini kuwa chanzo kikuu cha matatizo haya ni kutoeleweka kwa dhana nzima ya burudani hususan filamu, kutothaminiwa kwa filamu na kwa serikali kutokuwa na kipaumbele katika tasnia ya filamu katika mipango ya maendeleo ya nchi yetu.

Ingawa jamii na viogozi wa nchi yetu hawawezi kukwepa lawama kwa maendeleo hafifu ya sekta ya filamu na burudani kwa ujumla wake, wasanii, waandaaji na watendaji wengine katika sekta hii wanastahili kulaumiwa zaidi kwa kuwa hawafanyi jitihada za kutosha katika kuelimisha na kuwaelewesha wananchi juu ya dhana ya burudani (filamu), mchango wake katika uchumi, ajira na umuhimu wake katika kusimulia hadithi zetu.

Sekta hii inahitaji jitihada za kimtandao za ushawishi na utetezi. Hapana shaka jitihada hizi zikiwepo zitasaidia sana kuelekeza nguvu, kasi na ari zaidi iliyopo sasa katika jamii yetu kwenye maendeleo ya Sekta ya filamu.

Nimekuwa nikiipiga kelele Serikali kila mara kwa kuonekana kama imejitoa kwenye masuala yanayohusu filamu japo ina chombo kinachohusika na Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza, lakini hii imekuwa ikidhihirishwa na kuonekana kwa watu wachache tu wanaomiliki soko la filamu huku serikali ikiwa haiambulii chochote na wala haioneshi kushtuka.

Uhakika nilionao ni kwamba, hata kama Serikali ikijiondoa katika kuhudumia sekta ya filamu kivitendo, lakini haipaswii kujiondoa katika kudhibiti shughuli na soko la filamu, ikiwemo kufuatilia kwa makini data za mauzo ya filamu, kuwa na sera maalum ya filamu, kujenga miundombinu ya kimasoko na kuwa na chombo maalum cha kusimamia mambo haya. Hainiingii akilini kwa dola kuacha kufanya haya!

Kwa tathmini yangu, sekta ya filamu na burudani kwa ujumla ina udhaifu mkubwa sana katika ushawishi na utetezi. Wakati sekta hii ndiyo yenye matatizo ya kutoeleweka na kutothaminiwa, jambo ambalo sisi tulio ndani ya sekta yenyewe tunalifahamu vyema, ni aghalabu sana kukuta washiriki, wadau wa sekta hii au watu tuliowapa dhamana (viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania, TAFF) wakifanya jitihada za dhati za ushawishi na utetezi. Wote tuko kimyaa, tumenywea! Cha ajabu tukikutana wenyewe kwa wenyewe kwenye vikao vyetu, kwenye mitandao ya jamii kama facebook tunaelezana matatizo yetu, jinsi tunavyotaabika, jinsi tunavyopuuzwa, baada ya vikao tunaachana kila mmoja akiendelea na shughuli zake, hakuna kinachoendelea!

Jambo moja kubwa nakubaliana nalo ni kwamba mengi ya matatizo yetu makubwa katika tasnia ya filamu yako nje ya uwezo wetu kuweza kuyamaliza, japo binafsi nimekuwa natoa makala katika magazeti na kuyasema haya ninapoalikwa kwenye vituo vya televisheni, lakini bado haitoshi kufikisha ujumbe mbali zaidi. Wakati mwingine nadhani labda kudharaliwa kwa muda mrefu kwa sekta hii kumetufikisha mahali hata sisi wenyewe tukaanza kuona ni sawa sekta kudharauliwa, kupuuzwa na kudhalilishwa. Iweje sekta ya filamu ndiyo iwe kimbilio la watu waliokosa kazi za kufanya au walioshindwa masomo? Kwa kweli kazi iliyo mbele yetu katika maendeleo ya shughuli za filamu bado ni kubwa.

Kwa nini hatuna Taasisi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayohudumia Filamu? Ieleweke kuwa hapa kuna watendaji au wahusika wengi na wa aina tofauti: Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, hali kadhalika mashirika na makampuni yaliyo katika sekta binafsi. Na hata Wasanii pia wanahusika.

Kwa kweli wahusika ni wengi, lakini inavyoonekana hasa kwa upande wetu tulio ndani ya sekta hii, hatuna malengo ya aina moja, madhumuni wala majukumu mahsusi. Ingawa aina ya matatizo inafanana kwa wahusika wote, lakini inavyoonekana hata tuliowakabidhi jukumu la kutusimamia ndani ya sekta ya filamu (TAFF) hata majukumu yao hawayafahamu, au hawayatekelezi kwa kiwango kinachotakiwa, au hawayatekelezi kabisa. Wanafurahia kuitwa viongozi wa taasisi ya filamu na kukutana na wakubwa bila kujua majukumu yao!

Nadhani kuna umuhimu wa kukumbushana, kueleweshana na kuzinduana ili kazi iendelee na kasi iongezeke vinginevyo tutaendelea kulalamika kutengwa huku tukiendelea kuwafaidisha wachache na sisi kufa masikini.

Kwa ujumla ipo hali dhahiri ya kuwepo kwa uelewa mdogo wa dhana ya nzima ya burudani katika nchi hii. Hali hii inapunguza hamasa au mwamko kwa wasanii, watayarishaji filamu na hata viongozi kutafakari na kujishughulisha na mambo mengi ya sanaa hii.

Ni bahati mbaya sana hata viongozi na watendaji wanaopewa dhamana katika wizara husika na idara zake wamo katika kundi hili la kukosa uelewa kuhusiana na thamani, mchango kiuchumi na dhana nzima ya burudani. Hawa ndio wenye fursa ya kufanya maamuzi ya hatma ya maendeleo ya sekta yetu. Inashangaza hata Wabunge wanaohubiri ajira kwa vijana, ambao wanapaswa kuwa makini katika kutafakari mipango ya Serikali, hutumia muda mchache sana kuongelea burudani japo wanakiri kuwa ina mchango mkubwa sana katika nchi hii.

Hii ni ishara kuwa hawana uelewa wa kutosha wa dhana na dhima ya fani nyingi za burudani. Hamasa au mvuto wao kwa fani hizo ni mdogo. Hali hii ni hivyo hivyo kwa watunga sera ambao wanatoa kipaumbele cha chini sana kwa sekta hii. Kama nilivyosema hawa ndio wapitisha maamuzi. Huenda kosa sio lao. Ni sisi tulio ndani ya Sekta hii ambao hatuwapi fursa ya kuelewa au kujenga hamasa kutokana na harakati zetu za ushawishi na utetezi wa sekta ya filamu na burudani kwa ujumla.

Japo iliwahi kutangazwa kuwa serikali inatoa misamaha kwa vifaa vya uzalishaji filamu, lakini kumekuwepo ukiritimba na usumbufu mkubwa pindi unapoingiza vifaa hivyo, ni kama hakuna misamaha inayotolewa, na hii ni sababu inayotokana na Serikali na watu wengine kutotambua kikamilifu kuwa filamu pia ni sekta inayoweza kuchangia kwa kwango kikubwa mno uchumi wa nchi hii. Inaweza na tayari inaingizia nchini fedha za kigeni moja kwa moja au kupitia sekta nyingine kama vile utalii na biashara ya mahoteli na mabaa.

Zipo nchi, kama vile Afrika ya Kusini, ambazo zinapata mabilioni ya dola za Kimarekani kila mwaka kutokana na sekta ya filamu. Masuala ya msingi hapa yanayohitaji ushawishi ni mahitaji zaidi ya nyenzo na fedha kwa Sekta ya filamu, hasa ikishakuwa rasmi.

Pia wasanii na watendaji wengine wanapaswa kupatiwa mafunzo, kwangu mafunzo ndiyo kitu cha kwanza muhimu kwa mtu yeyote yule katika kumuongezea stadi zake za utendaji. Kwa jumla kuna upungufu mkubwa wa mafunzo ya fani mbalimbali za sanaa, ikiwemo filamu. Wasanii wengi wanajifunza kwa kuiga wenzao. Ingawa hii ni moja ya njia za kujifunza, tatizo lake ni kuwa huchukua muda mrefu na haina hakika kama kinachoigwa ni sahihi au la.

Tutafute njia nyingine nzuri za kuwapatia mafunzo wasanii wetu na watendaji wengine ndani ya sekta ya filamu, kwani mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ni kwa waliohitimu kidato cha nne na kuendelea. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chenyewe huchukua walio na sifa za kusomea shahada. Lakini kwa kuwa vijana wengi wenye vipaji katika nchi hii hawakubahatika kwenda sekondari, na wangependa kujiendeleza katika sanaa ili wapate staid, sijui tunawasaidiaje?

Kwa kupuuza hili matokeo yake ni wasanii wengi kufanya kazi bila kupitia mafunzo maalum, sekta hii kuonekana ni ya watu walioshindwa masomo au kukosa kazi za kufanya, na kwa hiyo ufanisi wa kazi umekuwa wa chini mno. Lakini hata kwa waliokwenda vyuoni, tuna tatizo pia la mafunzo yatolewayo kutokidhi kikamilifu mahitaji ya wasanii kutokana na upungufu wa walimu waliobobea, vifaa vya mafunzo na vitabu.

Kwa hiyo eneo hili la mafunzo linahitaji msukumo siyo tu wa kuongeza nafasi bali pia ubora wake. Ushawishi kwa uongozi na wamiliki wa asasi za mafunzo ni muhimu. Ni muhimu pia kushawishi asasi au watu binafsi kuanzisha mafunzo kwa ajili ya fani ya filamu kama tunataka kuendelea.

Kwa kweli bado tuna changamoto kubwa. Tunatakiwa kuacha kulumbana na kuangalia namna nzuri ya kuandaa sera itakayotuongoza kwenye mafanikio ya soko la filamu. Tuunganishe nguvu zetu, ujuzi wetu na elimu yetu ili jitihada zetu ziwe na mafanikio kwa maslahi yetu na vizazi vyetu vijavyo.

Chanzo: http://bishophiluka.blogspot.com/

Asante!

Posted by Bongo Film Data Base on 2:13 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for BISHOP HILUKA ; MATATIZO HAYA MPAKA LINI?

Post a Comment

LETS HOOK UP

.

.
.
slide

SIRI YA MTUNGI PHOTO CAPTION


Recently Commented

ALBUM YA BONGOFILM

SIMULIZI ZILIZOBAMBA KWENYE KURASA ZA KIJAMII

TAKE ONE -HBABA NA FLORA INTERVIEW

2009 Bongofilmdatabase. All Rights Reserved. - Designed by Oscar kwa ushirikiano wa SimplexDesign