MJUE VILIVYO MAMA TECLA MJATA..



TECLA Mjata ni mwanamama mwenye kipaji cha hali ya juu katika uigizaji, ni mtu ambaye anaubeba uhusika wake ipasavyo huku akionesha kazi yake ya sanaa ya maigizo kwa kukupa uhalisia wa tukio lenyewe.
Pamoja na umahiri katika kuigiza kwenye filamu na michezo ya redio, Mjata ambaye anapenda kujitambulisha kama mama Mjata amepitia katika milima na mabonde ya maisha halisi hususani ya uigizaji.
Anasema, alianza fani ya uigizaji kati ya miaka ya 1955 na 1960 akiwa mwanafunzi ambapo alikuwa akishiriki katika michezo ya kuigiza wakati wa Siku ya Wazazi iliyokuwa ikifanyika kila mwaka shuleni kwao na hiyo ilitokana na fani ya uigizaji kuwa kwenye damu.
Baada ya kumaliza elimu ya msingi na baadaye chuo cha uwalimu mwaka 1963, alipangiwa kazi ya kufundisha Shule ya Msingi Kwamagome.
Mjata alifundisha shule mbalimbali baadhi yake zikiwa ni Kwamsangazi, Magunga Mombo na baadaye alihamishiwa Dar es Salaam ambapo alipangiwa kufundisha Shule ya Msingi Kisutu na kufuatia na Olimpio.
” Nikiwa ni mwalimu niliendelea na sanaa ya uigizaji kwa kuwafundisha wanafunzi michezo mbalimbali au hadithi, lakini mapenzi yangu zaidi yalikuwa ni mimi mwenyewe kuigiza na si vinginevyo.”
“Sababu hasa ya kuingia kwenye sanaa hii ilikuwa michezo ya kuigiza iliyokuwa ikifanyika Radio Tanzania (kwa sasa TBC1 Taifa), ambapo wasanii kama Ibrahimu Raha (Mzee Jongo), Hamisi Tajili, Tunu Mrisho (Mama Hambiliki), Ali Keto (Pwaguzi au Matuga) na Nyakomba walinivutia na mimi nikasema nikipata nafasi nitafanya vizuri zaidi.”
” Nilianza kuigiza michezo ya redio katika kipindi cha Mahoka na Pwagu na Pwaguzi ambapo tulikuwa tunaigiza vituko vilivyotokea mitaani. Kama utakumbuka yule mtoto aliyeng’olewa meno na koleo za baiskeli basi nilikuwa ni mimi.
” Pamoja na uwezo huo kumpendezesha baba yangu aliyekuwa mwalimu, marehemu Davis Salimu, lakini kila wakati alikuwa akinionya kuwa tabia ya kuigiza mambo ya watu tunaweza kupata madhara, lakini mimi nilihakikisha kuwa hilo halitatokea.
Anasema, mwaka 1975 akiwa mwalimu aliomba kwenda kusoma Chuo cha Ualimu cha Chang’ombe kwa sasa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DECE) ambako kulikuwa na kitengo cha sanaa za maonesho (theatre art), muziki na sanaa ya uchoraji.
” Mimi nikachagua kusoma sanaa za maonesho ambapo nilisoma kwa mwaka mmoja na nilifaulu na kupata alama A. Matokeo hayo yalinifanya nijisemee kuwa sasa hapa nimefika. ” Nikaacha kufundisha shule za msingi na kuanza kufundisha Shule ya Sekondari Zanaki nikiwa Mwalimu Msaidizi Daraja la Pili, nikafurahia ambapo nilikuwa nikifundisha masomo ya Kiswahili na Siasa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha tatu.
“Lakini tatizo la wizara (Wizara ya Elimu), somo la sanaa za maonesho halikuwekwa kwenye mtaala, nililazimika kuifanya kazi hii kama Party time (kwa muda wa zaida), ukishamaliza kufundisha Kiswahili, au Siasa saa 10 wakati huo umechoka,”alisema Mjata.
Alikuwa akisubiri wakati wanafunzi wengine wanakwenda kwenye netiboli basi yeye anachukua kikundi chake kwenda kukifundisha. Hali hiyo ilimfanya akabiliane na changamoto kubwa katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi.
Mjata ambaye mtaani kwake maeneo ya Ubungo ni maarufu kama Shangazi au Bibi Tunu anasema: “Baada ya muda nikaomba kazi ya Ofisa Utamaduni baada ya nafasi kuwa wazi katika Wilaya ya Ilala.”
Alifanya kazi hiyo kwa miaka mitatu akiwa Ofisa Michezo na Utamaduni Wilaya ya Ilala na baada ya kufanya vizuri akahamia Temeke ambapo nako alifanya kazi hiyo kwa miaka mitatu kabla ya kuamua kuingia kwenye uigizaji.
Mjata alizaliwa Julai 2, 1946 akiwa ni mtoto wa tano wa familia ya Davis Salimu na Josephine Mchirwa. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alikwenda kujiendeleza Chuo cha Mpwapwa, Dodoma.
Akizungumzia changamoto za Ofisa wa Michezo na Utamaduni, Mjata anasema kuwa haikumuwia vigumu sana kushughulikia migogoro katika michezo husani ya Simba na Yanga. “Nilikuwa Ofisa Utamaduni ambaye alikuwa akizielewa vizuri Simba na Yanga, ikitokea migogoro au suala la kurekebisha Katiba basi tulikuwa tunayamaliza kwa njia nzuri tu.”
Anasema kuwa baada ya kuona tangazo la Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC), aliamua kuingia kwenye fani ambayo alikuwa anaipenda.
Akiwa TFC, aliigiza filamu yake ya kwanza iitwayo Fimbo ya Mnyonge sehemu ya pili ikiwa ni mwendelezo wa filamu ya kwanza ya Fimbo ya Mnyonge au Yombayomba. Hapo kazi yetu ilikuwa ni kupeleka ujamaa vijijini.
Katika filamu hiyo aliigiza kama Katibu wa Kijiji. “Enzi hizo makamera makubwa na mataa na hata kama mnaigiza saa sita mchana lazima mataa yawashwe,” anasema.
” Kwa bahati mbaya, mimi naita bahati mbaya kwani filamu ile ambayo iliandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu na TFC ilikamilika, eti serikali ikaona yale yaliyozungumzwa ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea yamepitwa na wakati. Ikaishia kuwekwa maktaba.
“Nilisikitika sana, ilikuwa filamu yangu ya kwanza, lakini lugha iliyotumika mle, matukio ndani ya filamu ile mpaka leo yanatokea na pengine yangekuwa mafunzo, ukiachilia mbali vijiji vya ujamaa na maduka ya kupanga foleni ambayo hayapo,” anasema.
Baada ya mwaka mmoja aliigiza filamu ya Harusi ya Mariam iliyoigizwa katika mandhari ya Korogwe ambapo baadhi ya walioigiza pamoja anamkumbuka Profesa Amandina Lihamba na marehemu Godwin Kaduma na hapo aliigiza kama shangazi yake Mariam.
“Ile filamu iliongozwa na Mmarekani (Roney Mafiel) na ilipokwenda kuhaririwa Ulaya alinipigia simu akisema ‘mama Mjata umefanya wonders (maajabu)’ kwani kila anayeiangalia filamu ile aliifurahia. Nilifurahi sana maana kuna wengi walisema nisingeweza kufanya kitu,” anasema.
Ilipokamilika kuna watu wengine walidai waliiga uigizaji wa Nigeria, lakini Mjata anasisitiza kuwa waliigiza kwa mazingira ya kienyeji kuanzia nyumba, mavazi na vyombo na hakukuwa na ghorofa.
Anasema filamu hiyo ilipelekwa kwenye tamasha lililofanyika Ouagadougou, Burkina Faso ambako ilishinda tuzo ya filamu bora iliyochezwa katika mandhari ya kijijini.
” Mwaka uliofuata ilipelekwa katika tamasha la Afrika lililofanyika Harare, Zimbabwe na huko ikapata tuzo na safari hii ilikuwa ni tuzo ya mama Mjata kama muigizaji hodari mwanamke.
“Ile kauli ya kusema umepata tuzo, ilinifurahisha kiasi cha kwamba lile donge nililokuwa nalo kusema filamu nimeitengeneza sipati chochote hata ofisi hainipandishi cheo kwa kazi nilizofanya.
“Nikamwambia bosi wangu waweza kufanya chochote na hapo akanitaka niipeleke mwenyewe kwenye tamasha la filamu za Afrika lililofanyika Japan,” anasema.
Mjata anasema akiwa bado mtumishi wa TFC, kazi ya kutengeneza filamu ilianza kuzorota kwani filamu nyingi zilizokuwa zikitengenezwa zilikuwa za mashirika kama vile Misitu. Anasema lengo la TFC haikuwa kutengeneza filamu za kampuni, bali filamu za Kitanzania ili Watanzania wasiagize filamu kutoka nchi yoyote ile, lakini lengo hilo halikutimizwa.
Kwa maoni yake lengo la TFC lilitimizwa katika filamu za Fimbo ya Mnyonge, Harusi ya Mariam, Watoto Wana Haki na Umati.
” Kuingia kwa televisheni, TFC ikashindwa kuendana na teknolojia hiyo na hapo watu wakapunguzwa kazi, nikiwemo mimi na baada ya mwaka mmoja kampuni ilikufa kabisa.
” Baada ya kupunguzwa nilikuwa na uwezo wa kurudi kuwa Ofisa Utamaduni, au hata uwalimu, lakini niliona niendelee na shughuli za uigizaji,” anasema.
Anasema yule Mmarekani alikuja nchini kwa mara nyingine na akaigiza filamu ya Maangamizi ambayo pia ilikuwa na mafanikio.
” Ukiangalia filamu nilizoigiza kama Harusi ya Mariam, Matumaini na Maangamizi, kitu nilichokuwa najivunia ni kuigiza na professional (wataalamu) maprofesa wa chuo kikuu, kama Amandina Lihamba, mama Mrama na marehemu Kaduma, nilijiona kuwa nina kiwango.
Hali hiyo ilimfanya aone hakuna haja ya kurejea kwenye ualimu kwani alikuwa na uhakika wa kupata kazi.
Anasema walimu wa chuo kikuu kama marehemu Chambwili Kazi na Gonche Matelego (Katibu Mkuu wa Basata) walimtumia katika miradi kadhaa ambayo ilikuwa ikipitia vyuoni na kupitia wao aliigiza filamu nyingi.
Baadhi ya filamu alizoigiza ni Suturday Morning ya Mtitu, Trip to Amerika, Wakati na Divorce za JB. Pia ameigiza katika filamu ya Mlima wa Kalole ya Irene Sanga, Asha ya Deo Shija, Simu ya Kifo ya Triypod Media, The Will ya Neema Kambona, Nimechoka ya Maria Sarungi na Hukumu ya Tunu ya Benchmark ambayo mpaka sasa watu wanataka irudiwe.
Mafanikio
Anasema kama isingekuwa sanaa ya uigizaji, asingeweza kuishi jijini Dar es Salaam hasa sasa hivi kwa kuwa ni mjane.
” Bila filamu ningekimbia mji, lakini nashukuru naendesha maisha yangu bila matatizo na nimefanikiwa kujenga nyumba ambayo nimeipangisha mbele na mimi naishi nyumba ya uwani,” anasema.
Mwaka 2002, Mfuko wa Utamaduni ulimpa tuzo kwa kuthamini mchango wake katika kuelimisha.
Anasema filamu ya Harusi ya Mariam na Maangamizi, zimemfanya ajione ‘yuko juu’ hasa kutokana na miaka ya 1992 kutumiwa na wanafunzi kujifunzia Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hekaheka za kazi Anasema akiwa na kundi la Mambo Hayo anakumbuka sana mchezo aliouigiza wa ‘Usilolijua ni kama usiku wa giza.’ ” Mchezo huo ulinifanya nikipanda basi nalipiwa nauli, au utakuta mtu anakufuata na kukuambia nashukuru bwana umenisafishia nyumba yangu, maana mchezo ukianza mama mkwe wangu anaondoka. Ilikuwa ni kama nawasema watu,” anasema.
Mjata ameamua kuwa msanii wa kujitegemea baada ya kubaini dhuluma na malipo finyu kwenye vikundi.
“Kwenye vikundi kuna ugumu mkubwa na ndio maana havidumu, kunakuonea kwingi, msanii anapata kiasi kidogo hata kama wewe ndiye uliyeinua huwezi kupata hela na viongozi ndio wananufaika.
“Tangu niingie kwenye fani hii sijawahi kupata matatizo, kwa bahati nzuri mume wangu (Marehemu David) alikuwa anaelewa, kama nakwenda redio saa 10 jioni mpaka saa mbili usiku, ananivumilia, nikirudi ndio tutaanza kupika basi tutapika, hata mikoani aliniamini.ni ufinyu wa mawazo, pale hakifanyiki kitu chochote, na kama watu wanafanya ujinga wao basi itakuwa wakati wa kazi na si wakati tunaigiza.
Ulinganisho wa maadili na taaluma
Mjata anasema kumekuwa na tofauti kati ya sanaa ya sasa na enzi zao, anasema: “Sisi zamani tulikuwa tunaigiza kwa upenzi kwamba ninapenda kazi, kipato kilikuwa ni majaliwa, ukipewa kitu asante lakini jambo la msingi lilikuwa uigize na ukifanikiwa kuelimisha jamii basi inakuwa furaha yako.
” Lakini kwa sasa mtu anaingia katika uigizaji fedha mbele, na hii ndiyo inafanya leo aigize na kesho anajiita ‘director’ au ‘producer’, lakini wanajua kuwa ‘director’ anatakiwa asome kiasi gani na aelewe nini, unajua mambo ya kamera, utunzi, kumuelekeza mtu, je, anajua ratiba ya kazi?” Anahoji.
Kumbukumbu
Mjata anasema maisha yake katika uigizaji hatasahau mchezo wa redio wa ‘Nani alaumiwe’ ambao aliutunga mwenyewe na alitaka kukomesha tabia za akinababa ambao wanawazunguka wake zao na kutembea na ndugu wa mkewe ambaye anaishi naye.
Akizungumzia uigizaji uliokuwa mgumu kwa upande wake ni pale mwongozaji wa filamu alipomtaka wapigane kweli kweli na msanii mwenzake Mama Bishanga.
” Nafasi hiyo niliiona shida sana na kitaalamu hairuhusiwi, angenitia kofi, mimi nisingekubali ndipo nilipomshauri kwanini mimi nisitake kumkata nywele mama Bishanga na kukawa na purukushani na ikawa hivyo,” anasema.
Akizungumzia michezo, Mjata anasema alikuwa mpenzi wa Yanga, sambamba na mume wake, lakini mwaka 1976 Simba ilipoifunga Yanga kwa mabao 6-0 ndipo alipohamia kushabikia timu ya Simba.
” Mimi nikuwa Yanga damu, mpaka khanga nilikuwa nanunua, lakini siku Yanga ilipofungwa mabao 6-0 na Simba na tuliporudi nyumbani, kile kitendo cha kucheza kipigo kile, kuliibuka malumbano na mume wangu sijawahi pata. Nikaona yanini togombane, tangu siku hiyo nikahamia Simba na nikawa nakwenda uwanjani hasa ukichukulia kuwa nilikuwa Ofisa Utamaduni.
Aidha, Mjata atavitiwa na kazi za wasanii Ndumbagwe Misayo ‘Thea’, Steven Charles ‘Kanumba’, Vicent Kigosi, ‘Ray’, Yvonne Ngatikwa ‘Monalisa’ na kuwa wasanii hao kwa sasa ameamua kufanya kazi na wanafanya kazi.
Kwa sasa Mjata ambaye anaigiza kwenye tamthilia inayoendelea TBC1 ya ‘Martini’, ana mtoto mmoja aitwaye Aneth na wajukuu watatu David, Achi, na Tecla ambao wawili wa mwisho wameonesha dalili ya kufuata nyayo za bibi yao.

Habari hii iliandikwa na Anastazia Anyimike wa Gazeti la Habari Leo na ilichapishwa katika gazeti hilo mwezi Januari mwaka 2010.
chanzo...bongo celebrity

Posted by bongofilmdatabase on 7:50 PM. Filed under , , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for MJUE VILIVYO MAMA TECLA MJATA..

Post a Comment

LETS HOOK UP

.

.
.
slide

SIRI YA MTUNGI PHOTO CAPTION


Recently Commented

ALBUM YA BONGOFILM

SIMULIZI ZILIZOBAMBA KWENYE KURASA ZA KIJAMII

TAKE ONE -HBABA NA FLORA INTERVIEW

2009 Bongofilmdatabase. All Rights Reserved. - Designed by Oscar kwa ushirikiano wa SimplexDesign