BISHOP: KWANINI NIGERIA IWE KIPIMO CHA FILAMU ZETU?
Posted by bongofilmdatabase
udaku
8:58 PM
Sekta ya filamu Tanzania kwa sasa inajulikana duniani licha ya matatizo
yake, licha ya mtayarishaji wa filamu wa Tanzania kuendelea kuishi
maisha yasiyo tofauti na mtu mwingine wa kawaida! Hali halisi ya soko la
filamu nchini inabana sana uwezekano wa kuibuka kwa wasanii,
watayarishaji au waongozaji wapya...
Sidhani kama kuna mtu
atabisha kuwa filamu za kibongo ‘hazitesi’ katika ukanda wa Afrika
Mashariki na maeneo ya Maziwa Makuu. Filamu hizi zimesaidia kwa kiwango
fulani kuitangaza nchi hii, kuwatangaza wasanii wa nchi hii, lakini vipi
kuhusu maisha ya wasanii hawa? Je, wanapata stahili yao na wanaishi kwa
kutegemea filamu pekee?
Kinachosikitisha zaidi: utoaji wa hizi
filamu zetu imekuwa kama mchezo wa soka bila refa, sawa na mkutano bila
mwenyekiti, darasa bila mwalimu, au nyumba (familia) bila mzazi…
Wafanyabiashara wanaahidi milioni kumi na tano hadi ishirini na ushee
kwa sinema; watoaji sinema wanalipua kazi; waigizaji hawalipwi vizuri;
utengenezaji sinema unafanywa haraka haraka. Sinema zinatengenezwa kwa
wiki moja na zinatolewa ndani ya mwezi mmoja tu. Haraka haraka…
Wasanii wa filamu wanaigiza bila script wala mazoezi, watengenezaji
filamu wengi wanatumia mwanya huo kula uroda na wasichana wazuri wazuri
(ndiyo maana siku hizi kuwa miss ni kigezo kikubwa cha kupata nafasi ya
kucheza filamu, haijalishi kama una kipaji cha kuigiza au la), sinema
zinazotolewa nchini eti zinalinganishwa na za Wanaijeria! Tangu lini
sinema za Wanaijeria zikawa kipimo cha filamu?
Kwa nini tufuate
nyayo za Nollywood katika kuzalisha sinema zetu? Kwa kipi hasa? Hii
inatufanya kusimulia hadithi zao; angalia sinema zetu zinavyosimulia
uchawi, zinavyosimulia mapenzi au mikasa ya kijamii utagundua hilo.
Tunaiga hadithi zao, namna yao ya uchezaji, sinema zao ambazo nyingi
zimekuwa zikiigwa kutoka mataifa ya Magharibi na India.
Hivi
Watanzania tumelogwa? Hii ni kwa Watanzania wote. Kwanini hatupendi/
hatununui sinema zinazotolewa na Watanzania wenzetu? Kisa? Hazituvutii.
Moja ya sababu ni kwamba zinatengenezwa vibaya kwa kulipuliwa. Lakini
kwa nini hata sinema zinazotengenezwa vizuri bado hatuzinunui? Kwa nini
hatuzifurahii? Kwa nini hatuzitolei maoni na kuzitangaza? Tunachoweza ni
kuziponda tu! Hivi hatudhani kuwa hiyo ndiyo njia kuu itakayotufanya
tuendelee kama wenzetu, tunaowaona Miungu kutuzidi?
Kwa upande
wa waandaaji wa filamu tukumbushane kwamba sinema ni sanaa inayochukua
muda. Hatuwezi kutengeneza sinema ikakamilika ndani ya mwezi mmoja tu.
Tujipe muda katika kuifanya kazi kwa ufanisi zaidi. Ingawa wapo
wanaosema kuwa sababu ya kufanya kazi haraka haraka ni kutokana na
matatizo ya pesa ambapo mtu huhitaji kupata pesa haraka ili atatue
matatizo yake. Lakini tunasahau kuwa ukitoa kazi nzuri yenye ubora hukaa
na huuzika miaka nenda miaka rudi, tofauti na kazi zetu ambazo baada ya
wiki mbili zinakuwa hazina tena soko.
Tukumbushane kujipa muda
katika uandaaji wa filamu zetu: Mwezi mmoja wa mikutano kupanga mambo
(wapi itapigwa picha, nani atafanya nini, waigizaji watatoka wapi,
watafanya nini), mwezi mwingine kupanga usanii (mazoezi ya waigizaji,
mazingira yao), mwezi mwingine wa kupiga picha. Baada ya miezi mitatu,
mingine miwili ya kuhariri na kusahihisha makosa.
Ndipo sasa
kifuate kipindi cha kuitangaza kusudi iuzwe. Ukichunguza sana utagundua
kuwa sinema haiwezi kumalizika chini ya miezi sita kwa mazingira ya
Tanzania. Ndiyo maana wenzetu wanatoa sinema moja tu kwa mwaka lakini
pesa wanazopata wanakula kwa miaka kibao. Sisi tunatoa sinema kila mwezi
lakini pesa yake ni ya kujikimu tu.
Ni wakati sasa umefika tushirikiane, tuzichangamkie na tuangalie sinema zetu, tuzifurahie na tupeane moyo…
Posted by bongofilmdatabase
on 8:58 PM.
Filed under
udaku
.
You can follow any responses to this entry through the
RSS 2.0