BISHOP HILUKA ; MATATIZO HAYA MPAKA LINI?
mtandao, slide 2:13 PM
SEKTA ya filamu ni moja ya
sekta ambazo zimezongwa na matatizo makubwa. Tathmini nyingi zilizofanyika na
zinazoendelea kufanyika zinabaini kuwa chanzo kikuu cha matatizo haya ni
kutoeleweka kwa dhana nzima ya burudani hususan filamu, kutothaminiwa kwa filamu
na kwa serikali kutokuwa na kipaumbele katika tasnia ya filamu katika mipango
ya maendeleo ya nchi yetu.
Ingawa jamii na viogozi wa
nchi yetu hawawezi kukwepa lawama kwa maendeleo hafifu ya sekta ya filamu na
burudani kwa ujumla wake, wasanii, waandaaji na watendaji wengine katika sekta
hii wanastahili kulaumiwa zaidi kwa kuwa hawafanyi jitihada za kutosha katika
kuelimisha na kuwaelewesha wananchi juu ya dhana ya burudani (filamu), mchango
wake katika uchumi, ajira na umuhimu wake katika kusimulia hadithi zetu.
Sekta hii inahitaji
jitihada za kimtandao za ushawishi na utetezi. Hapana shaka jitihada hizi
zikiwepo zitasaidia sana kuelekeza nguvu, kasi na ari zaidi iliyopo sasa
katika jamii yetu kwenye maendeleo ya Sekta ya filamu.
Nimekuwa nikiipiga kelele
Serikali kila mara kwa kuonekana kama imejitoa kwenye masuala yanayohusu filamu
japo ina chombo kinachohusika na Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza, lakini
hii imekuwa ikidhihirishwa na kuonekana kwa watu wachache tu wanaomiliki soko
la filamu huku serikali ikiwa haiambulii chochote na wala haioneshi kushtuka.
Uhakika nilionao ni kwamba,
hata kama Serikali ikijiondoa katika kuhudumia sekta ya
filamu kivitendo, lakini haipaswii kujiondoa katika kudhibiti shughuli na soko
la filamu, ikiwemo kufuatilia kwa makini data za mauzo ya filamu, kuwa na sera
maalum ya filamu, kujenga miundombinu ya kimasoko na kuwa na chombo maalum cha
kusimamia mambo haya. Hainiingii akilini kwa dola kuacha kufanya haya!
Kwa tathmini yangu, sekta
ya filamu na burudani kwa ujumla ina udhaifu mkubwa sana katika ushawishi na utetezi. Wakati sekta hii ndiyo
yenye matatizo ya kutoeleweka na kutothaminiwa, jambo ambalo sisi tulio ndani
ya sekta yenyewe tunalifahamu vyema, ni aghalabu sana kukuta washiriki, wadau wa sekta hii au watu
tuliowapa dhamana (viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania, TAFF) wakifanya jitihada za dhati za ushawishi na
utetezi. Wote tuko kimyaa, tumenywea! Cha ajabu tukikutana wenyewe kwa wenyewe kwenye
vikao vyetu, kwenye mitandao ya jamii kama facebook tunaelezana
matatizo yetu, jinsi tunavyotaabika, jinsi tunavyopuuzwa, baada ya vikao
tunaachana kila mmoja akiendelea na shughuli zake, hakuna kinachoendelea!
Jambo moja kubwa nakubaliana
nalo ni kwamba mengi ya matatizo yetu makubwa katika tasnia ya filamu yako nje ya
uwezo wetu kuweza kuyamaliza, japo binafsi nimekuwa natoa makala katika
magazeti na kuyasema haya ninapoalikwa kwenye vituo vya televisheni, lakini
bado haitoshi kufikisha ujumbe mbali zaidi. Wakati mwingine nadhani labda
kudharaliwa kwa muda mrefu kwa sekta hii kumetufikisha mahali hata sisi wenyewe
tukaanza kuona ni sawa sekta kudharauliwa, kupuuzwa na kudhalilishwa. Iweje
sekta ya filamu ndiyo iwe kimbilio la watu waliokosa kazi za kufanya au
walioshindwa masomo? Kwa kweli kazi iliyo mbele yetu katika maendeleo ya
shughuli za filamu bado ni kubwa.
Kwa nini hatuna Taasisi na
Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayohudumia Filamu? Ieleweke kuwa hapa
kuna watendaji au wahusika wengi na wa aina tofauti: Serikali Kuu, Serikali za
Mitaa, Mashirika ya Umma, hali kadhalika mashirika na makampuni yaliyo katika
sekta binafsi. Na hata Wasanii pia wanahusika.
Kwa kweli wahusika ni
wengi, lakini inavyoonekana hasa kwa upande wetu tulio ndani ya sekta hii, hatuna
malengo ya aina moja, madhumuni wala majukumu mahsusi. Ingawa aina ya matatizo
inafanana kwa wahusika wote, lakini inavyoonekana hata tuliowakabidhi jukumu la
kutusimamia ndani ya sekta ya filamu (TAFF) hata majukumu yao hawayafahamu, au hawayatekelezi kwa kiwango
kinachotakiwa, au hawayatekelezi kabisa. Wanafurahia kuitwa viongozi wa taasisi
ya filamu na kukutana na wakubwa bila kujua majukumu yao!
Nadhani kuna umuhimu wa
kukumbushana, kueleweshana na kuzinduana ili kazi iendelee na kasi iongezeke
vinginevyo tutaendelea kulalamika kutengwa huku tukiendelea kuwafaidisha
wachache na sisi kufa masikini.
Kwa ujumla ipo hali dhahiri
ya kuwepo kwa uelewa mdogo wa dhana ya nzima ya burudani katika nchi hii. Hali
hii inapunguza hamasa au mwamko kwa wasanii, watayarishaji filamu na hata viongozi
kutafakari na kujishughulisha na mambo mengi ya sanaa hii.
Ni bahati mbaya sana hata viongozi na watendaji wanaopewa dhamana katika
wizara husika na idara zake wamo katika kundi hili la kukosa uelewa kuhusiana
na thamani, mchango kiuchumi na dhana nzima ya burudani. Hawa ndio wenye fursa
ya kufanya maamuzi ya hatma ya maendeleo ya sekta yetu. Inashangaza hata Wabunge
wanaohubiri ajira kwa vijana, ambao wanapaswa kuwa makini katika kutafakari
mipango ya Serikali, hutumia muda mchache sana kuongelea burudani japo wanakiri kuwa ina mchango
mkubwa sana katika nchi hii.
Hii ni ishara kuwa hawana
uelewa wa kutosha wa dhana na dhima ya fani nyingi za burudani. Hamasa au mvuto
wao kwa fani hizo ni mdogo. Hali hii ni hivyo hivyo kwa watunga sera ambao
wanatoa kipaumbele cha chini sana kwa sekta hii. Kama nilivyosema hawa ndio wapitisha maamuzi. Huenda kosa sio lao. Ni sisi tulio
ndani ya Sekta hii ambao hatuwapi fursa ya kuelewa au kujenga hamasa kutokana
na harakati zetu za ushawishi na utetezi wa sekta ya filamu na burudani kwa
ujumla.
Japo iliwahi kutangazwa
kuwa serikali inatoa misamaha kwa vifaa vya uzalishaji filamu, lakini
kumekuwepo ukiritimba na usumbufu mkubwa pindi unapoingiza vifaa hivyo, ni kama
hakuna misamaha inayotolewa, na hii ni sababu inayotokana na Serikali na watu
wengine kutotambua kikamilifu kuwa filamu pia ni sekta inayoweza kuchangia kwa
kwango kikubwa mno uchumi wa nchi hii. Inaweza na tayari inaingizia nchini
fedha za kigeni moja kwa moja au kupitia sekta nyingine kama vile utalii na biashara ya mahoteli na mabaa.
Zipo nchi, kama vile Afrika ya Kusini, ambazo zinapata mabilioni ya dola za Kimarekani
kila mwaka kutokana na sekta ya filamu. Masuala ya msingi hapa yanayohitaji
ushawishi ni mahitaji zaidi ya nyenzo na fedha kwa Sekta ya filamu, hasa
ikishakuwa rasmi.
Pia wasanii na watendaji
wengine wanapaswa kupatiwa mafunzo, kwangu mafunzo ndiyo kitu cha kwanza muhimu
kwa mtu yeyote yule katika kumuongezea stadi zake za utendaji. Kwa jumla kuna
upungufu mkubwa wa mafunzo ya fani mbalimbali za sanaa, ikiwemo filamu. Wasanii
wengi wanajifunza kwa kuiga wenzao. Ingawa hii ni moja ya njia za kujifunza,
tatizo lake ni
kuwa huchukua muda mrefu na haina hakika kama kinachoigwa ni sahihi au la.
Tutafute njia nyingine
nzuri za kuwapatia mafunzo wasanii wetu na watendaji wengine ndani ya sekta ya
filamu, kwani mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ni kwa
waliohitimu kidato cha nne na kuendelea. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chenyewe huchukua walio na sifa za kusomea shahada.
Lakini kwa kuwa vijana wengi wenye vipaji katika nchi hii hawakubahatika kwenda
sekondari, na wangependa kujiendeleza katika sanaa ili wapate staid, sijui
tunawasaidiaje?
Kwa kupuuza hili matokeo
yake ni wasanii wengi kufanya kazi bila kupitia mafunzo maalum, sekta hii
kuonekana ni ya watu walioshindwa masomo au kukosa kazi za kufanya, na kwa hiyo
ufanisi wa kazi umekuwa wa chini mno. Lakini hata kwa waliokwenda vyuoni, tuna
tatizo pia la mafunzo yatolewayo kutokidhi kikamilifu mahitaji ya wasanii
kutokana na upungufu wa walimu waliobobea, vifaa vya mafunzo na vitabu.
Kwa hiyo eneo hili la
mafunzo linahitaji msukumo siyo tu wa kuongeza nafasi bali pia ubora wake.
Ushawishi kwa uongozi na wamiliki wa asasi za mafunzo ni muhimu. Ni muhimu pia
kushawishi asasi au watu binafsi kuanzisha mafunzo kwa ajili ya fani ya filamu kama tunataka kuendelea.
Chanzo: http://bishophiluka.blogspot.com/