ELIMU KWA WASANII WA FILAMU NCHINI
habari, slide, udaku 9:14 AM
Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) na asasi ya Gaba Arts mapema wiki hii wameendesha semina fupi
kwa Wasanii wa filamu ili kuwajengea weledi katika eneo la uandishi bora wa miswada
ya sinema (script writing).
Semina hiyo
iliyoendeshwa kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa kwenye Ukumbi wa BASATA ilijikita
katika maeneo ya namna ya kuendeleza wazo hadi sinema ya kusisimua, namna ya
kufikia hisia za watazamaji,ujenzi mzuri wa matukio,kutengeneza wahusika na mfumo
wa hadithi, Mwanzo, kati na hitimisho.
Akitoa mada kwenye
programu hiyo maalum, Mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts James Gayo alisema kuwa,
muda umefika sasa kwa wasanii wa filamu kusaka maarifa ili kutengeneza sinema
zenye visa vipya, zenye weledi na zisizosukumwa na matakwa au maelekezo ya
wasambazaji.
“Wenzetu kutoka nje
wanatamani sana kupata vitu kutoka Afrika vyenye kuzungumza uhalisia wa maisha
ya kwetu, wanataka kuona vitu vipya hivyo, katika uandishi wa muswada wa sinema
suala la uhalisia na visa vyenye utofauti ni la msingi sana” alisisitiza Gayo.
Alizidi kueleza kuwa
watazamaji wa sinema (filamu) huwa wana kawaida ya kuchoka pale wanapolishwa
visa vya aina moja muda wote na akaonya kuwa kama wasanii hawatajikita katika
kubuni visa vipya na vyenye kugusa uhalisia wa maisha yao wadau watasusia
kununua.
“Ikiwa tutaendelea
kutengeneza filamu zisizo na weledi, zenye visa vilevile na zenye kusukumwa na
wasambazaji au haja ya kuchuma fedha za haraka tu watu watatuchoka na baadaye soko
litakufa” alionya Gayo.
Gayo ambaye amepitia
mafunzo ya utengenezaji filamu katika mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani
alitaja sifa za muswada (script) bora kuwa ni pamoja na kubeba wazo
linalozalika kwenye jamii, visa vyenye uhalisia na vipya, utengenezaji mzuri wa
wahusika na sifa zingine nyingi.
Kwa upande wake
msanii wa mashairi Mrisho Mpoto ambaye alikuwa miongoni mwa waliohudhuria
semina hiyo alisema kuwa, wasanii wa filamu wanahitaji kusaidiwa kwani kwa sasa
soko la filamu limekuwa la kitumwa na lenye kuburuzwa na matakwa ya wasambazaji
bila weledi.
Akihitimisha programu
hiyo, Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego alishauri wasanii wa filamu
kujipanga kushirikiana na wasomi wenye weledi katika maeneo yao ili kuzalisha
kazi zenye weledi la ubora.
E
“Tuna wataalam wengi
katika Sanaa, wamebanana na mambo mengi lakini ni vema wasanii tukawatumia na
kushirikiana nao katika kuboresha kazi zetu” alisisitiza Materego.
Captions
1.
Mkurugenzi wa asasi ya Gaba Arts James
Gayo akisisitiza jambo wakati akitoa mafunzo kwa wasanii wa filamu juu ya Stadi
za Uandishi wa Miswada ya Sinema (Script) kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika
kila wiki makao ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
2.
Bw. Gayo akifafanua hatua katika
uandishi wa muswada bora wa filamu (script)
3.
Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche
Materego akitoa ufafanuzi kuhusu uandishi wa Miswada bora ya simema (Scripts)
kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
4.
Mtunzi na mwongozaji wa Sinema wa
Kundi la maigizo la Jakaya Theatre linalorusha michezo yake kila Jumamosi
kupitia ITV, Chedieli G. Senzighe akichangia kwenye mjadala.
5.
Msanii wa Sanaa ya ushairi Mrisho
Mpoto naye alitoa mchango wake na kuuliza maswali kadhaa juu ya uandishi bora
wa miswada katika sinema.
6.
Sehemu ya Wasanii waliohudhuria elimu
hiyo wakifuatilia moja ya filamu zilizotengenezwa kutokana na muswada (script)
makini.
7.
Wadau waliohudhuria programu hiyo
wakifuatilia kwa makini.
Na. mwandishi wetu
Na. mwandishi wetu