Mmiliki wa blogi ya U Turn Mange Kimambi, matatani
mpya, mtandao, slide, udaku 7:47 PM
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni,
jijini Dar es Salaam, limekiri kumshikilia kwa saa kadhaa kwa mahojiano
mmiliki wa ‘blog ya Uturn’, Mange Kimambi, kwa madai ya kumhusisha
muigizaji maarufu nchini, Vicent Kigosi au Ray, na kifo cha nguli wa
tasnia hiyo, Steven Kanumba, ‘The Great’.
Akizungumza na Tanzania Daima jana,
Kamanda wa Polisi mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles
Kenyella, alisema Ray alikwenda kulalamika kwenye kituo hicho, kuhusu
maneno yaliyoandikwa kwenye mtandao huo akiomba msaada wa jeshi hilo.
“Ninathibitisha kwamba huyo dada
tulimshikilia hapa kwetu tangu jana (juzi), tumemwachia leo (jana), kwa
sababu dhamana ni haki yake, ila tunaendelea na upelelezi, maana
anadaiwa kutuma taarifa kwenye mtandao akimhusisha Ray na kifo cha
Kanumba.
“Hiyo blog haijahalalishwa kutoa
taarifa za kukashifu na kuwadhalilisha watu… ameandika skandali kwa Ray,
tukiiachia hii, maneno hayo yanaweza kuonekana halali na kuleta maafa
katika jamii, hasa kwa huyo anayetajwa,” alisema Kamanda Kenyella na
kuongeza kwamba kesi iko mahakamani, hivyo si vema kuingilia upelelezi.
Kwa upande wake, Ray aliyekuwa rafiki
wa karibu wa marehemu Kanumba, alisema kitendo hicho kinahatarisha
maisha yake, hivyo ameapa kulishughulikia suala hilo, huku akisisitiza
kwamba suala hilo linamvunjia heshima na kumharibia kazi yake.
“Hiki sio kitu cha kweli, Kanumba ni
mdogo wangu na tumetoka mbali kimaisha, huyu dada Mange Kimambi simjui…
ameandika uongo, sijajua hizi habari amezipata wapi hii ni kutaka
kunishushia heshima katika jamii.
“Uigizaji ndiyo kazi yangu, kwa hiyo anapoandika na kuweka kwenye
intaneti inayosomwa dunia nzima, anataka kuniharibia kazi yangu? Anataka
kuniharibia maisha? Anataka kunipotezea mashabiki?
“…Unategemea watu wanioneje? Hili sitaliacha, nitalifanyia kazi na
kulifikisha mahakamani ili iwe fundisho kwa wanaotumia kalamu zao kutaka
kuwaharibia wengine, chochote kitakachonikuta nitadili na huyo mama…
haya ni maisha, nitaendelea kuvumilia Mungu yupo,” alisema Ray
anayetamba kwenye medani ya filamu ndani na nje ya nchi.
Juhudi za kumpata Mange, aliyewahi
kuandaa shindano la urembo la Dar Indian Ocean 2006 na kumwibua Wema
Sepetu, hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopatikana.
Chanzo Tanzania Daima,Jukwaa huru.